Nimekuwa nawaza sana kuhusu maisha siku za hivi karibuni, na kwa ujumla ni kwamba Mungu anatupenda sana, tena sana. Ukitafakari jinsi mtu anavyoweza kukukosea, na jambo la kwanza ukajiuliza, “nimemfanyia nini huyu mtu?”. Yaani unajaribu kutafuta sababu ya hicho kitu anachokuumiza nacho. Na mara nyingi ni mambo madogo tu, kama chuki, wivu na mengine mengi tu.
Hebu sasa fikiria, Mungu anavyotupenda. Aliamua kumtoa Yesu pale msalabani. Yaani Yesu Kristo akapigwa, akateswa, akajeruhiwa, akatemewa mate, akavuliwa nguo akabaki uchi, na aibu yote, akachomwa mkuki ubavuni, akavikwa kofia ya miiba, akapigiliwa misumari, akanyimwa maji wakati alipopatwa na kiu, akapigwa ngumi za kutosha, akachapwa mijeredi mgongoni. Sasa katika kipindi chote hicho alikuwa na uwezo wa kuagiza majeshi kutoka mbinguni walete moto na kuangamiza wale watesi wake. Lakini akavumilia.
Yesu alivumilia mateso kwa sababu ya UPENDO alionao kwa wanadamu, kwa mimi na wewe. Yaani kwa lugha nyingine, hakusema, “nimewafanyia nini hawa watu mpaka waniue?”. Alipokeakikombe chake kamili cha mateso, na alibeba msalaba wake mpaka akatundikwa juu ya huo msalaba.
Sasa mtu wa namna hiyo, anajitolea uhai wake, bila mimi na wewe kuingia gharama yoyote ile. Yaani kazi yangu mimi na wewe ni kumwamini TU. Yaani kuamini tu. Kwa nini watu hatutaki zawadi ya BURE kabisa ya uzima wa milele? Yohana 3:16 inasema, “Kwa maana jinsi hii, Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa mwanae wa pekee, ili kila mtu asipotee, bali awe na uzima wa milele”. Na hakika hakuna upendo mkuu zaidi ya mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya mwingine.
Nakusihi ndugu, hebu fikiria ni namna gani unaweza kumpokea huyu Yesu leo kabla haijawa “TOO LATE”. Na ikishakuwa “TOO LATE”, maana yake hakuna nafasi ya pili tena. Maana ukishakufa, kinachofuata ni hukumu tu. Na kama CV yako haina msingi wa Yesu Kristo, basi itakuwa ni hasara ya milele. Kama ni ku-bet, ni bora ubet maisha yako na YESU, halafu usikilizie maisha yatakuaje.
Napoandika huu ujumbe leo, Yesu anaweza kurudi na kunyakua kanisa lake wakati wowote. Kwa yeyote ambaye hajampokea, hii siku itakuwa ya uchungu, majuto, kilio na kusaga meno. Lakini bahati mbaya, maneno haya haya ndio yatamhukumu na kumwambia, “ulifahamu ukweli lakini ulipuuza”.